Haya ni kwa mujibu wa Seyed Mohammad Moojani, mkuu wa kikundi cha kazi cha Qur'ani cha kamati ya kitamaduni na elimu ya makao makuu ya Arbaeen.
Akizungumza na IQNA siku ya Jumatatu, alitoa orodha ya maqari au wasomaji Qur'ani. Orodha hiyo inajumuisha Wairani 98 na raia wa kigeni 34 kutoka nchi 14, kama vile Afghanistan, Tajikistan, Nigeria, India, na Pakistan.
Shughuli za msafara huo zitaanza Agosti 14, zikiendelea kwa siku 12, Moojani alisema. Wasomaji Qur'ani wa kiume na wa kike pamoja na wanachama wa vikundi vya Tawasheeh watakuwa na programu mbalimbali kwenye njia tofauti kuelekea Karbala, aliongeza. Programu hizo zitahitimishwa kwa viikao vya Qur'ani huko Karbala katika mkesha wa Arbaeen, aliongeza.
"Kwa kuzingatia matukio ya hivi karibuni huko Palestina na Gaza, programu za Qur'ani za mwaka huu zinazingatia suala la Palestina na kuwakumbuka mashahidi wa Gaza, haswa Shahidi Ismail Haniyeh," ameongeza.
Maadhimisho ya Arbaeen hufanyika siku ya 40 baada ya Ashura, ukumbusho adhimu wa kuuawa shahidi Imam Hussein (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) ambaye aliuawa shahdi na jeshi katili la la Yazid katika vita vya Karbala mwaka 61 Hijria sawa na 680 Miladia.
Kila mwaka mamilioni ya Mashia na pia idadi kubwa ya wasiokuwa Mashia humiminika katika mji Karbala nchini Iraq, mji ulipo Haram Tukufu ya Imam Hussein (AS) ili kushiriki katika shughuli za maombolezo. Wafanya ziara, hasa kutoka Iraq na Iran, husafiri mamia ya kilomita kwa miguu hadi mji mtakatifu wa Karbala. Arbaeen ya mwaka huu inatarajiwa kuanguka mnamo Agosti 25, kulingana na kuonekana kwa mwezi.
Harakati ya mapambano ya Imam Hussein (AS) dhidi ya dhulma na ufisadi wa utawala wa Bani Umayya ilijaa hamasa, kujitolea na kusabilia kila kitu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, haki na uadilifu, na kwa sababu hiyo imegusa sana nyoyo za Waislamu na hata wapenda haki na kweli wasio Waislamu. Harakati hiyo ya Imam Hussein (AS) inaendelea kuibua vuguvugu na hamasa ya aina yake ndani ya nafsi za wapenzi wa mtukufu huyo.
3489488